Virusi vya Corona: Misiba ya watu maarufu iliyoibua gumzo la corona Tanzania

Haki miliki ya pichaMLIMA WA MOTO
Image captionMchungaji Getrude Lwakatare ambaye pia alikuwa mbunge wa viti maalum nchini Tanzania
Ndani ya kipindi cha wiki tatu zilizopita watu kadhaa maarufu nchini Tanzania kutoka Jaji Mkuu mstaafu, waziri mpaka viongozi wa dini wamefariki.
Japo sababu ya vifo vyao kutosemwa ama kuwa ni tofauti na corona kumekuwa na mjadala wa namna vilivyotokea ghafla na kwa kuongozana na pia juu ya hatua za tahadhari ambazo zimekuwa zikichukuliwa kwenye mazishi yao.
Mchungaji Getrude Lwakatare, ambaye alikuwa mchungaji mkuu wa Kanisa la Mlima wa Moto jijini Dar es Salaam na Mbunge wa Viti Maalumu nchini Tanzania aliaga dunia Aprili 20 jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa familia yake, kifo chake kilisababishwa na shinikizo la damu na matatizo ya moyo. Siku moja baadaye, Spika wa Bunge Job Ndugai akatangaza kuwa mazishi yake yatasimamiwa na serikali na kuwa yatahudhuriwa na watu wasiozidi 10.
Japo haikusemwa kuwa ni corona, ila ni utaratibu wa serikali kuongoza mazishi ya watu waliofariki kwa virusi hivyo na kuzuia idadi ya waombolezaji kwa uchache unaowezekana.
Siku chache baadae, Aprili 25 aliyewahi kuwa mbunge wa kisiwa cha Mafia Abdulkarim Shah alifariki dunia katika hospitali moja jijini Dar es Salaam na kuzikwa asubuhi ya siku iliyofuata na watu wachache.
Coronavirus
Banner
Aprili 27, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara (Kusini mwa Tanzania) Evod Mmanda alifariki dunia. Akithibitisha taarifa za kifo chake Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Sulemani Jafo alisema Mmanda alilazwa hospitali kwa siku mbili kabla kufikwa na mauti na alikuwa akikabiliwa na "changamoto za upumuaji."
Mazishi ya Mmanda yalifanyika siku iliyofuatia yakisimamiwa na serikali huku ndugu zake 10 tu wakiruhusiwa kushiriki.
Tarehe 27 Aprili pia ilishuhudia majaji wawili wastaafu nchini humo wakifariki, Jaji Ali Haji Pandu ambaye aliwahi kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na moja ya waasisi wa chama cha CUF na Jaji Mussa Kwikama ambaye alikuwa kiongozi mwandamizi wa chama cha ACT Wazalendo.
Siku hiyohiyo Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro Isihaka Sengo alifariki dunia hospitalini.
Siku iliyofuata mazishi yake ambayo yalikuwa yamepangwa na familia yalisitishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akisema marehemu alionesha dalili za virusi vya corona, na baadae mazishi yake yalisimamiwa na serikali na kuhudhuriwa na ndugu wachache.
Jaji Mkuu wake Mstaafu Jaji Augustino RamadhaniHaki miliki ya pichaNMG
Image captionJaji Mkuu Mstaafu Jaji Augustino Ramadhani aliaga dunia Aprili 28
Tarehe 28 Aprili Tanzania ilimpoteza Jaji Mkuu wake Mstaafu Jaji Augustino Ramadhani. Taarifa rasmi za Mahakama na Serikali ni kuwa Jaji Ramadhani alikuwa akisumbuliwa na saratani kwa zaidi ya miaka miwili na alipelekwa hospitali siku chache kabla ya kifo chake baada ya kuzidiwa.
Siku moja baadaye, Aprili 29 mbunge wa Sumve Richard Ndassa alifariki dunia baada ya kuugua ghafla, japo ugonjwa uliopelekea umauti wake haukutajwa.
Gazeti la The Citizen la nchini Tanzania pia liliripoti kuwa baada ya kifo chake hoteli aliyokuwa akikaa mbunge huyo ilinyunyiziwa dawa na hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia kwa muda.
Unawezaje kunawa mikono licha ya upungufu wa maji?
Ijumaa ya Mei Mosi Watanzania waliamka na taarifa ya Tanzia kutoka kwa rais John Magufuli akitangaza kifo cha aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Augustine Mahiga.
Taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa mwanadiplomasia huyo nguli aliugua ghafla alfajiri ya siku hiyo nyumbani kwake mjini Dodoma na alipofikishwa hospitali alikuwa ameshafariki.
Hicho kilikuwa ni kifo cha tatu cha mbunge katika kipindi cha chini ya wiki mbili. Hali hiyo ililazimu chama kikuu cha Upinzani nchini humo Chadema chini ya mwenyekiti wake Freeman Mbowe kuwataka wabunge wake kutokuhudhuria bungeni na kujitenga karantini kwa siku 14.
Chama hicho pia kimetoa rai ya bunge kuahirishwa kwa siku 21, lakini mpaka sasa vikao vinaendelea na rais Magufuli ameagiza wabunge hao walosusia vikao kutolipwa posho zao.
Peter MitimingiHaki miliki ya pichaMITIMINGI/FACEBOOK
Image captionMchungaji Maarufu wa Kanisa la Ghala la Chakula cha Uzima Peter Mitimingi
Usiku wa Mei 3, Mchungaji Maarufu wa Kanisa la Ghala la Chakula cha Uzima Peter Mitimingi alifariki dunia baada ya kuugua ghafla.
Mitimingi alikuwa maarufu kwa mahubiri yake ya mitandaoni nchini humo ambayo yalikuwa yakilenga nyanja mbalimbali za kimaisha kuanzia mahusiano, masomo mpaka ujasiriamali.
Usiku wa Mei 4, mwanasheria na mwanasiasa maarufu Tanzania Dkt Masumbuko Lamwai pia alifariki ghafla.
Taarifa zilizothibitishwa na familia yake ni kuwa Dkt Lamwai aliumwa na kuzidiwa ghafla na alipokimbizwa hospitali madaktari walithibitisha kuwa ameshafariki.
Lamwai alikuwa ni miongoni mwa wanasiasa machache wa mwanzo wa upinzani na alishinda ubunge kwa tiketi ya upinzani mwaka 1995. Pia alikuwa wakili maarufu na mhadhiri mwandamizi wa Sheria.
Usiku wa kuamkia leo Jumatano Mei 6 Shehe maarufu nchini Tanzania Suleiman Kilemile pia amefariki dunia.
Mwanazuoni huyo wa kiislamu hivi karibuni alirekodiwa akiwataka waislamu kuchukua tahadhari na kuwataka wenye nacho kutoa sadaka ya sabuni misikitini ili watu wanawe kwa maji na sabuni kama wanavyoshauri wataalamu wa afya.
'Sio wote waliokufa ni corona'
Serikali ya Tanzania imetoa tahadhari kuwa si kweli watu wote wanaofariki katika kipindi hichi ni kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.
Rais John Magufuli akilihutubia taifa siku ya Jumapili alisisitiza hilo na kusema haiwezekani wote wanaokufa kuwa na corona na kuwa kuna magonjwa mengine pia.
"…japo siyo vizuri kutoa taarifa za watu, lakini Jaji Ramadhani kwa mafano, amesumbuliwa muda mrefu na kansa, hata baba yangu alifariki kwa kansa. Tulihangaika na Jaji Ramadhani India na mwishoni hapa tukampeleka mpaka Nairobi...haiwezekani kila anayekufa ni corona tu."

Post a Comment

0 Comments