Virusi vya Corona: Wiki moja bila takwimu mpya za corona Tanzania, nini kimetokea?

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania
Jumatano wiki hii imetimu wiki moja toka Tanzania kutoa takwimu za mwisho za ugonjwa wa virusi vya corona nchini humo.
Hali hiyo inatokea wakati serikali ya nchi hiyo ikiwa inakosolewa juu ya namna inavyolishughulikia janga la corona.
Usiri wa taarifa ni moja ya maeneo ambayo wapinzani na wanaharakati wa ndani na nje ya nchi hiyo wamekuwa wakilalamikia.
Mpaka sasa taarifa rasmi ni kuwa, nchi hiyo imethibitisha wagonjwa 480 na vifo 10, pamoja na watu 167 kupona.
Ni dhahiri kuwa katika kipindi cha wiki moja iliyopita kuna mabadiliko kwenye takwimu hizo, japo hayajawekwa wazi na serikali.
Pia, hakuna takwimu mpya, mambo kadhaa kuhusu mwenendo wa korona yametokea nchini humo katika kipindi hicho cha wiki moja na haya ni baadhi:

Je, serikali imesema nini kuhusu tuhuma za usiri?

Alhamisi ya wiki iliyopita, yaani siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Tanzania kutoa takwimu mpya, Waziri wa Afya wa nchi hiyo alikanusha bungeni kuwa serikali inafanya usiri katika kutoa takwimu.
"Waziri Mkuu kaongea jana, mimi naongea…mwanzoni (mlikuwa mnasema) kwanza watu wenyewe wachache. Sasa tumetoa (mnasema) tumeshinda nchi zote za Afrika Mashariki. Hivi tungekuwa tunaficha tungetoa takwimu hizi ambazo tunaonesha Tanzania tuna wagonjwa wengi kuliko nchi nyengine za Afrika Mashariki. Tusingetoa hizo takwimu. Kwa hiyo hakuna usiri, tunazitoa kadri tunavyozipata kutoka maabara," alisema Waziri Mwalimu.
Bi Mwalimu hata hivyo aliliambia bunge kuwa hakukuwa na ulazima wa kutoa taarifa kila siku.
"Wataalamu wameniambia, 'Waziri huna haja ya kutoa takwimu kila siku. Sharti la kwanza la WHO (Shirika la Afya Duniani) lilikuwa ni kutoa taarifa ya kwanza ya kwamba tumepata case (mgonjwa) ya kwanza Covid-19 Tanzania', na taarifa hiyo tumetoa."
Wakati akizungumza bungeni Tanzania ilikuwa juu ya Kenya kitakwimu, lakini kutokana na ukimya wa wiki moja, huku Kenya ikiendelea kuripoti takwimu mpya, kwa sasa Kenya imethibitisha wagonjwa 580.
coronavirus
Life under lockdown divider
Rais Magufuli atilia mashaka ufanisi wa maabara, uchunguzi kufanyika
Siku ya Jumapili, rais Magufuli alimuapisha waziri mpya wa Katiba na Sheria Dkt Mwigulu Nchemba, na katika hotuba yake kwa taifa, aliagiza uchunguzi kufanyika katika maabara kuu ya taifa hilo ambayo imekuwa ikitumika kupima sampuli za corona.
Magufuli alieleza kuwa aliagiza sampuli za Wanyama na matunda kupewa majina ya binadamu na umri kisha kupelekwa ili zipimwe bila wataalamu wa maabara hiyo kujua na matokeo yakarudi kuwa baadhi ya sampuli hizo zimekutwa na maambukizi ya corona.
"…Lazima ugundue kuna mambo ya ajabu yanafanyika nchi hii. Ama wahusika wa maabara wamenunuliwa na mabeberu, ama hawana utaalamu jambo ambalo si kweli kwa kuwa maabara hii imetumika sana katika magonjwa mengine. Ama zile sampuli zinazoletwa maana vifaa vyote vinatoka nje, hivyo lazima kuna kitu fulani kinafanywa," alisema Magufuli.
Magufuli amesema kutokana na taarifa hizo anaamini kuna watu ambao walipewa majibu yasiyo sahihi.
"Lazima kuna watu wameambiwa positive lakini si wagonjwa wa corona, na inawezekana wengine wakafa kwa hofu."
Jambo hili linaweza kuwa ni moja ya sababu kuu ya kutotolewa kwa takwimu mpya kufikia sasa.
Waziri wa Afya wa Tanzania
Image captionWaziri wa Afya wa Tanzania Ummy Mwalimu
Tayari waziri Ummy Mwalimu amewasimamisha kazi Mkurugenzi wa maabara hiyo Dkt. Nyambura Moremi na Meneja wake wa Udhibiti wa Ubora Jacob Lusekelo na kuunda jopo la wataalamu kuwachunguza.

Chama kikuu cha upinzani chasusia vikao vya Bunge

Ijumaa ya wiki iliyopita, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani katika Bunge la Tanzania na Mwenyekiti wa chama cha Chadema Freeman Mbowe aliwataka wabunge wa chama chake kutokuhudhuria vikao vya Bunge vinavyoendelea na badala yake kujitenga karantini kwa wiki mbili.
Hatua hiyo ya chama hicho imejiri baada ya vifo vitatu vya wabunge chini ya kipindi cha wiki mbili. Hata hivyo vifo vya wabunge hao wote kutoka chama tawala cha CCM havijathibitishwa kuwa vimetokana na corona.
Hatua hiyo ya upinzani imekosolewa vikali na rais Magufuli ambaye aliagiza wasilipwe posho kwa kususia vikao.
Spika wa Bunge hilo Job Ndugai pia amemkosoa Mbowe kwa kusema hana mamlaka ya kuamuru wabunge wasusie vikao. Pia amewaagiza wabunge hao ikiwemo Mbowe kurejesha pesa za posho ya vikao ambayo tayari walishalipwa, na kuhakikisha kuwa wanapimwa ugonjwa wa Covid-19 kabla ya kurejea Bungeni baada ya wiki mbili la sivyo hawatapokelewa.
MakondaHaki miliki ya pichaMAKONDA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda jana aliwapatia wabunge waliopo katika mkoa huo saa 24 kurejea bungeni ama la watakamatwa na kurejeshwa Dodoma.
Wabunge kadhaa wa upinzani walijitokeza mitandaoni na kutangaza kuwa wapo jijini humo na kumuonya Makonda kuwa hana uwezo wa kuwakamata. Saa 24 hizo zinatimia mchana wa leo.

'Maiti zisizikwe usiku'

Jambo moja ambalo limezusha hofu nchini Tanzania wakati huu wa mlipuko wa corona ni namna serikali ilivyokuwa ikishughulikia mazishi ya watu ambao inaaminika wamekufa kutokana na maambukizo ya corona ama kuonesha dalili za ugonjwa huo kabla ya kufariki.
Video za siri zimetanda mitandaoni zikionesha mazishi hayo ambayo yalikuwa yakifanyika kwa tahadhari kubwa za kiafya na chini ya ulinzi.
Jumapili iliopita serikali ya nchi hiyo kupitia Wizara ya Afya ililitolea muongozo jambo hilo na kusema kuwa hakuna sababu ya maiti kuzikwa usiku ama gizani.
"Katika kipindi hiki, tunaelekeza maafisa afya na waganga wakuu wa wilaya na mikoa kuhakikisha familia zinashirikishwa kikamilifu na bila hofu au haraka katika kuandaa na kufanya mazishi kwa heshima zote za utu," imeeleza sehemu ya taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Abel Makubi.
Pia unaweza kutazama:
Coronavirus: Utajuaje kuwa umeathirika na virusi?


Post a Comment

0 Comments